Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bangura aunga mkono vikwazo dhidi ya waasi DRC

Bangura aunga mkono vikwazo dhidi ya waasi DRC

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya ukatili wa ngono kwenye maeneo ya migogo Zainab Hawa Bangura amesema anaunga mkono vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama dhidi ya vikundi vya waasi vya FDLR na M23 huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, DRC. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(SAUTI ASSUMPTA)

Taarifa ya Bi. Bangura iliyotolewa leo imesema kuwa vikwazo hivyo ni hatua ya awali ya kudhibiti vitendo vya ghasia zinazohusishwa na ukatili wa kingono zinazofanywa na vikundi hivyo vya FDLR na M23.

Halikadhalika ameunga mkono kutajwa bayana kwa Luteni Kanali Eric Badege na Jean-Marie Lugerero Runinga wa M23 kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na amesema kwamba kamati ya vikwazo ya Baraza la Usalama dhidi ya DRC imefungua njia ya kumulikwa kwa ukatili wa kingono kama kitendo cha uhalifu.

Bi Bangura amezitaka nchi wanachama kutekeleza wajibu wao katika kusimamia vikwazo hivyo ikiwemo marufuku ya safari na kuzuia mali za watuhumiwa. Halikadhalika ametaka mkutano wa kimataifa kwa nchi za maziwa makuu kupitia kamati ya pamoja ya ufuatililiaji wa mipaka iliyoko Goma kusaidia mamlaka za DRC kuzuia na kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ukatili wa kingono.