Mahitaji yazidi kuongezeka Syria

8 Januari 2013

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema mahitaji ya kibinadamu nchini Syria yanaongezeka, likitaja zaidi vyakula ambapo mikate na mafuta vimeadimika zaidi nchini humo.

Shirika hilo linasema kuwa kwa sasa linahudumia watu Milioni Moja na Nusu kila mwezi wakati linakadiria kuwa watu Milioni Mbili na Nusu ndio wanaohitaji msaada.

WFP imesema inashindwa kutoa msaada wake ipasavyo kutokana na kutokuwepo kwa washirika wa kusaidiana na kwamba kuna changamoto kubwa kufikia maeneo yaliyokumbwa na mzozo unaoendelea nchini humo.

Wakati hayo yakiendelea nchini Syria, wimbi kubwa la raia wengine wamendelea kumiminika katika nchi za jirani hatua ambayo inaongeza mzigo wa WFP kuwahudumia wakimbizi walioko katika nchi za Iraq, Jordan, Lebanon na Uturuki.