Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hotuba ya Assad inabomoa wala haijengi: Ban

Hotuba ya Assad inabomoa wala haijengi: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameeleza kusikitishwa kwake na hotuba ya jana ya Rais wa Syria Bashar Al Assad kwa wananchi wake ambayo amesema haichangii katika kumaliza machungu yanayokabili raia wa Syria bali inachochea ghasia zaidi.

Bwana Ban amekaririwa na Msemaji wake akieleza kuwa hotuba hiyo inakataa kwa kiasi kikubwa vipengele vya makubaliano ya Geneva ya mwezi Juni mwaka jana kuhusu kipindi cha mpito wa kisiasa na kuundwa kwa serikali ya mpito yenye madaraka kamili na inayoshirikisha wawakilishi wa wananchi wote.

Katibu Mkuu amesema kutokana na hali hiyo hakuna wakati wowote zaidi ya sasa ambapo Jumuiya ya Kimataifa inatakiwa kusaidia wasyria kujenga nchi  yao mapema iwezekanavyo mwaka huu na kuweka mazingira ambamo kwayo kila mwanachi atalindwa.

Amesema yeye anashikilia msimamo wake kuwa hakuna suluhisho la kivita kwa mgogoro wa Syria na kwamba Umoja wa Mataifa kwa upande wake utaendelea kushirikiana na washirika wote kuleta amani nchini humo