Helikopta mbili za MONUSCO zashambuliwa huko GOMA

28 Disemba 2012

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, DRC, MONUSCO umesema helikopta zake mbili zilishambuliwa Jumatano usiku kaskazini mwa mji wa Goma.

Taarifa ya MONUSCO inaeleza kuwa helikopta hizo zilikuwa katika safari zake za kawaida za kuthibitisha ubora wake wa kuruka ambapo moja ilishambuliwa huko Kibumba na nyingine Kanyamahoro, maeneo ambayo yote yanadhibitiwa na kundi la waasi la M23.

MONUSCO imesema mashambulizi hayo yaliripotiwa na watendaji wa kikosi cha pamoja cha kufuatilia usalama wa mipaka, JVM huko Goma.

Matumizi ya helikopta hizo ambazo sio za kijeshi ni kusafirisha watendaji wa Umoja wa Mataifa na raia kwa ajili ya matibabu.

MONUSCO imerejelea wito wake kuwa walinda amani wako katika eneo mahsusi wakifanya kazi yao ya amani na hivyo mashambulizi yoyote dhidi yao ni kitendo cha uhalifu. Imesema wahusika wa mashambulio hayo watashtakiwa na sheria itachukua mkondo wake.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter