Sudan Kusini yajumuishwa rasmi orodha ya nchi maskini duniani: UNCTAD

28 Disemba 2012

Taifa la Sudan Kusini lililopata uhuru wake mwaka 2011 limejumuishwa rasmi katika orodha ya nchi maskini duniani na kufanya idadi ya nchi hizo kufikia 49.

Shirika la Umoja wa Mataifa la biashara na maendeleo UNCTAD, limesema Sudan Kusini imejumuishwa tarehe 18 mwezi huu na hivyo ina haki ya kupata misamaha kadhaa ili iweze kuondokana na umaskini.

Misamaha hiyo ni pamoja na upendeleo wa biashara kwa mujib wa makubaliano na washirika wa  maendeleo ambazo ni nchi tajiri, misaada ya kigeni pamoja na ile ya kiufundi .

Sudan Kusini ilipata uhuru wake tarehe Tisa Julai mwaka 2011 kutoka Sudan baada ya miongo miwili ya vita kati  ya pande mbili hizo.

Nchi zinaweza kujikwamua na kuondoka katika orodha hiyo ya nchi maskini ambapo kwa mujibu wa UNCTAD, nchi tatu zimeshaondolewa ambazo ni Botswana mwaka 1994, Cape Verde mwaka 2007 na Maldives mwaka 2011.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter