Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama latoa tamko juu ya hali ya usalama huko Jamhuri ya Afrika ya Kati

Baraza la Usalama latoa tamko juu ya hali ya usalama huko Jamhuri ya Afrika ya Kati

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeelezea wasiwasi wake juu ya hali ya Usalama huko Jamhuri ya Afrika ya Kati na kushutumu vikali mashambulizi yanayoendelea kufanywa na kikundi cha waasi kiitwacho SELEKA kwenye miji mbali mbali nchini humo.

Taarifa ya Baraza hilo imekariri wajumbe wake wakisema kuwa kitendo hicho kinakwamisha makubaliano ya amani ya Libreville na kutishia pia usalama wa raia na utulivu wa nchi hiyo, huku wakisema wanaunga mkono mpango wa amani uliopitishwa na jumuiya ya nchi za Afrika ya Kati huko Nd’jamena tarehe 21 mwezi huu.

Wametaka waasi kusitisha mapigano, kuondoka katika miji waliyotwaa na kuacha kusonga mbele kueleka mji mkuu Bangui huku ikitaka pia pande husika kuheshimu haki za binadamu na kumaliza mzozo kwa njia ya amani.

Halikadhalika wamekumbusha wajibu wa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ya kusimamia utulivu na amani na kuhakikisha usalama wa raia.