Mtoto wa miaka 12 ashamirisha jitihada za mazingira Kenya: IFAD

26 Disemba 2012

Mpango wa mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya Kilimo, IFAD wa kufadhili miradi ya upandaji miti nchini Kenya umeanza kuzaa matunda ambapo tangu mwaka 2005 hadi sasa zaidi ya miche Milioni Moja imepandwa katika maeneo ya vyanzo vya maji kwenye miteremko ya mlima Kenya.

Miche hiyo inajumuisha miche Elfu Nne iliyopandwa na shule ya msingi Kambaru ambako mtoto Morris Kaboro mwenye umri wa miaka 12 ametumia pia ujuzi huo kumuelimisha babu yake ambaye awali alikuwa anakata miti kwa ajili ya kuni bila kufahamu madhara ya kitendo hicho.

Faith Livingstone kutoka mradi wa majaribio wa udhibiti wa rasilimali asili kwenye mlima Kenya anasema uhifadhi wa mazingra unasaidia kuboresha rutuba ya udongo.

"Rutuba ya udongo ni muhimu sana. Iwapo kuna mmomonyoko wa udongo wa mara kwa mara udongo unaporomoka na rutuba inapotea na hata kilimo kinakuwa hakina tija kwa wakulima, usalama wa chakula unakuwa unatishiwa na wakulima wanakuwa maskini. Na kadri wanavyokuwa maskini ndiyo kadri watakavyokata miti na inakuwa ni mzunguko wa matatizo.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud