Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uharibifu mpya wa makaburi ya kihistoria huko Timbuktu unasikitisha: UNESCO

Uharibifu mpya wa makaburi ya kihistoria huko Timbuktu unasikitisha: UNESCO

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Teknolojia, UNESCO Irina Bokova ameeleza kusikitishwa kwake na kubomolewa hivi karibuni kwa makaburi takribani matatu ya kihistoria katika mji wa Timbuktu nchini Mali.

Taarifa ya UNESCO imemkariri Bi. Bokova akisema kitendo hicho kimetokea wakati shirika lake limeanza kutekeleza wajibu wake kwa wananchi wa Mali tangu uharibifu wa kwanza uliofanyika mwezi Julai mwaka huu.

Amesema UNESCO ilipeleka mara mbili ujumbe wa dharura kutathmini uharibifu. Halikadhalika Kamati ya urithi wa dunia ya UNESCO ilipitisha azimio la kuanzisha mfuko maalum wa dharura wa kukarabati na kuhifadhi makaburi hayo na mengineyo ambayo ni utamaduni wa Mali.

Bi. Bokova ametaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kuhakikisha mali na maeneo hayo muhimu yanalindwa kwa kuwa ni alama muhimu za Mali.