Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miili ya askari wanne wa Urusi waliouawa huko Sudan yarejeshwa nyumbani: UNMISS

Miili ya askari wanne wa Urusi waliouawa huko Sudan yarejeshwa nyumbani: UNMISS

Miili ya askari wanne wa Urusi waliofariki dunia baada ya helikopta waliyokuwemo ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini, UNMISS kutunguliwa huko jimbo la Jonglei siku ya Ijumaa imesafirishwa leo kwenda nyumbani.

Ibada ya kuwaombea ilifanyika kwenye kituo cha UNMISS karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Juba.

Naibu Waziri wa ulinzi wa Sudan Kusini, Majak D'Agoot alitoa salamu za rambirambi za serikali kwa familia na serikali ya Urusi na kusema kuwa Sudan Kusini itachunguza kwa kina tukio hilo.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini Hilde F. Johnson alizungumzia mamlaka ya Umoja wa Mataifa kulinda raia jimbo la Jonglei na kuongeza kuwa walinda amani hao wa Urusi wamefariki dunia wakiwa kazini.

Ameunga mkono tamko la serikali ya Sudan Kusini la kuwasaka waliotekeleza kitendo hicho na kuwafikisha mbele ya sheria.