Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukeketaji wanawake ni kitisho kwa afya za wanawake: Ban

Ukeketaji wanawake ni kitisho kwa afya za wanawake: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezungumzia vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake ukiwemo ukeketwaji na kusema kuwa vitendo kama hivyo vinaweka hatarini afya za wanawake na wasichana wengi kote duniani.

Amesema afya za mamilioni ya wanawake na watoto duniani kote ziko hatarini na kwamba kuendelea kwa vitendo hivyo kunavunja haki zao za msingi.

Ban Ki-moon amesema hayo katika taarifa yake ya kupongeza kitendo alichosema cha kihistoria cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio linalotaka nchi wanachama kuchukua hatua madhubuti kuondosha vitendo vya ukeketaji wanawake na wasichana.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa wastani wa wanawake milioni 140 duniani kote wameathiriwa na vitendo vya ukeketaji na baadhi yao wamekumbwa na matatizo ya kiafya kutokana na kupoteza damu nyingi wakati utekelezaji wa tendo hilo.

Azimio hilo ambalo limedhaminiwa na robo tatu ya nchi wanachama ikiwemo kundi la nchi za Afrika, linalaani vitendo vyote vya ukeketaji na linataka kuwepo kwa shabaha ya makusudi kukabiliana na hali hiyo.