Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanajeshi wa DRC na waasi washutumiwa kwa kuhusika kwenye vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu

Wanajeshi wa DRC na waasi washutumiwa kwa kuhusika kwenye vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu

Umoja wa Mataifa unasema kuwa kulingana na uchunguzi lililoendesha limebainisha kuwa wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo pamoja na wapiganaji wa kundi la M23 walitekeleza vitendo vinavyokiuka haki za binadamu wakati wa mapigano ya kutaka kuudhibiti mji wa Goma ulio mashariki mwa nchi hiyo.

Vitendo hivyo vinaripotiwa kutekelezwa kati ya tarehe 20 na 30 mwezi Novemba kwenye mji wa Minova mkoani Kivu Kusini. Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa takriban wanawake 126 wakiwemo watoto 24 walikuwa wakubwa waathiriwa wa dhuluma za kimapenzi. Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Waliotenda hayo walikuwa ni wanajeshi wa jeshi la Congo na uhalifu huo unaonekana kutendwa wakati walikuwa wakirudi nyuma kutoka wakati wa mapigano mjini Goma na Sake. Makundi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa pia yamepokea madai ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu yakiwemo mauaji ya raia hasa eneo la Rutshuru ambayo ni ngome ya M23. Tuna wasi wasi mkubwa kutokana na visa hivi ambayo kwa mara nyingine vinavuruga maisha ya raia mashariki mwa DRC na tuna hofu kuwa kwa mara nyingine tena wanawake na wasichana wanalengwa na makundi kadha likiwemo jeshi la serikali ambalo linastahili kuwalinda. Tunazishauri pande zote kwenye mzozo kuheshimu haki za binadamu na sheria ya kimataifa. Hatua zaidi zitachukuliwa ili kutambua wahusika ili wafikishwe mbele ya sheria.