Mzozo wa Syria wazidi kuongezeka: UM waomba dola Bilioni 1.5 kusaidia wakimbizi

19 Disemba 2012

Idadi ya raia wa Syria waliopoteza makazi yao kutokanana mapigano yanayoendelea nchini mwao inatarajiwa kuongezeka na kufikia Milioni Nne katika nusu ya kwanza ya mwaka ujao.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa kati yao, Milioni Moja watakuwa wamekimbilia Jordan, Uturuki, Lebanon, Misri na idadi ya wakimbizi wa ndani itafikia Milioni Mbili.

Kwa mantiki hiyo basi Umoja huo utahitaji dola Bilioni Moja na Nusu kwa kipindi cha miezi sita ijayo kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya kibinadamu ya wakimbizi wa Syria.

Mratibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa kwa misaada ya kibinadamu nchini Syria, Radhouane Nouicer amesema mgogoro huo unazidi kupanuka na kuathiri raia nchini kote Syria.

Ghasia nchini Syria inaongezeka na hakuna eneo salama ambapo watu wanaweza kukimbilia kujihifadhi kwa kuwa maeneo yote kuna mapigano hata mji mkuu Damascus. Na zaidi ya yote ni kukata tamaa miongoni mwa raia wa Syria ambao wanazidi kuathiriwa na mgogoro huu. Ombi letu tulilowasilisha kwa serikali zote hii leo limejikita katika masuala ya kuokoa maisha mathalani chakula, malazi, afya, maji safi na salama pamoja na usafi. Mambo haya yote yanagharimu asilimia 80 ya bajeti yote.”

Wakati huo huo Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema nusu ya watu waliopoteza makazi yao nchini Syria kutokana na mgogoro unaoendelea ni watoto.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter