Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu laridhia tarehe 13 Februari kuwa siku ya Radio duniani

Baraza Kuu laridhia tarehe 13 Februari kuwa siku ya Radio duniani

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo limeridhia azimio la shirika   la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Teknolojia, UNESCO la kutaka tarehe 13 Februari ya kila mwaka kuwa siku ya kimataifa ya Radio duniani.

Tarehe 13 Februari mwaka 1946 ni siku ambayo Radio ya Umoja wa Mataifa ilianza kufanya kazi ambapo Baraza Kuu limetambua pia nafasi ya Radio katika kuwa na uwezo mkubwa wa kupasha habari idadi kubwa ya watu licha ya maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano.

Halikadhalika Baraza Kuu limepongeza jitihada za Radio ya Umoja wa Mataifa ya kuendelea kueneza vipindi vyake kwa lugha mbali mbali na kwamba ijitahidi kusambaza zaidi vipindi vyake maeneo mengi zaidi kwa kadri inavyowezekana.

Siku ya Kimataifa ya Radio inalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa baina ya watangazaji, na kuhamasisha vituo vikubwa vya radio na vile vya kijamii viendeleze haki ya msingi ya wananchi kupata taarifa na uhuru wa kujieleza kupitia radio.