Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fedha zaidi zahitajika kudhibiti Malaria: WHO

Fedha zaidi zahitajika kudhibiti Malaria: WHO

Shirika la afya duniani, WHO limesema dola Bilioni Tano zinahitajika kila mwaka kwa kipindi cha muongo mmoja ujao ili kuhakikisha tiba dhidi ya Malaria inapatikana duniani kote. Hata hivyo WHO imesema mpaka sasa ni nusu tu ya kiwango hicho ndicho kinapatikana na hivyo kukwamisha harakati za kupambana na ugonjwa huo.

Dkt. Richard Cibulskis mtaalamu kutoka WHO Geneva anasema jitihada zaidi zinatakiwa ili kufikia malengo.

Nchi 50 ndio ziko kwenye mwelekeo wa kufikia malengo ya kimataifa ya kupunguza Malaria kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2015. Hii ina maana ni nchi 50 kati ya 99 zinazokumbwa na Malaria. Mafanikio mengine ni ongezeko la watu wanaojitokeza kuchunguzwa malaria na vile vile wanaotumia tibaya Artemisinin. Hii ina maana watu wanapimwa na wanapata tiba.

Dkt. Cibulskis amesema iwapo usambazaji wa vyandarua utapungua na halikadhalika kasi ya kupulizia dawa, bila shaka kasi ya maambukizi ya malaria itareja kwa kasi kubwa zaidi.

Malaria ni tishio kwa nchi 14 duniani ambapo Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo zinazoongozwa kwa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara na India inaongoza kwa nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia.