Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM yapokea fedha za kufadhili huduma kwa waathiriwa wa kimbunga Bopha.

IOM yapokea fedha za kufadhili huduma kwa waathiriwa wa kimbunga Bopha.

Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM limepokea zaidi ya dola 700,000 kufadhili shughuli za misaada kwa waathiriwa wa kimbunga Bopha nchini Ufilipino, misaada ambayo ni pamoja na huduma za afya na malazi.

Kulingana na ripoti IOM kwa ushirikiano na idara ya kijamii na maendeleo DSWD juma hili ilitoa msaada wa makao ya dharura kwa familia 600 au watu 30,000 ambao wamekuwa wakiishi nje tangu tufani hiyo kupiga kisiwa na Mindanao tarehe nne mwezi huu.

Mkuu wa IOM nchini Ufilipino Jose Pimentel amesema ofisi yake inashirikiana na serikali ya nchi hiyo na ofisi ya Umoja wa Mataifa kuratibu misaada na kwamba msaada huo wa fedha kutoka Canada utasaidia kutimiza lengo lao.

Amesema wanashirikiana pia na sekta binfasi kuwasilisha misaada kwa wananchi huko Mindanao ambapo wameweka mfumo ambao kwao wahisani wadogo na wakubwa wanaweza kufuatilia kuona vile ambavyo misaada waliyotoa inatumika.

IOM inahitaji dola Milioni sita za kimarekani kati ya dola Milioni 65 zilizoombwa na Umoja wa Mataifa.