Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano kati ya WFP na Saudi Arabia waokoa maisha ya mamilioni

Ushirikiano kati ya WFP na Saudi Arabia waokoa maisha ya mamilioni

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP, Ertharin Cousin, amehitimisha ziara yake ya siku mbili huko Saudi Arabia na kusema kuwa ushirikiano kati ya pande mbili hizo umesaidia kuokoa maisha ya mamilioni ya watu wanaokabiliwa na njaa duniani kote.

Katika mazungumzo yake na Mwanamfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud, Bi Cousin amesema Saudi Arabia ilitoa ahadi ya kihistoria ya mchango wa dola Milioni 500 kusaidia mamilioni ya watu waliokuwa na uhaba wa chakula mwaka 2008.

Hii ilikuwa ni zara ya kwanza ya Mkuu huyo wa WFP kwenye eneo la ghuba tangu achukue wadhifa huo mwezi Aprili mwaka huu.

Saudi Arabia huipatia WFP zaidi ya tani Elfu Nne za tende kila mwaka ambapo tangu kuanzishwa kwa WFP miaka ya 1960, nchi hiyo imeshatoa zaidi ya dola Bilioni Moja kusaidia kupambana na njaa.