Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usafirishaji haramu wa binadamu wakumba zaidi watoto: UM

Usafirishaji haramu wa binadamu wakumba zaidi watoto: UM

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa vitendo vya usafirishaji watoto duniani vimeongezeka ambapo asilimia 27 ya waathirika wa vitendo vya usafirishaji wa binadamu duniani kote ni watoto.

Ripoti hiyo ni matokeo ya utafiti uliofanywa kati ya mwaka 2007 na 2010 na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na udhibiti wa madawa ya kulevya na vitendo vya uhalifu, UNODC, ambapo kiwango hicho kimeongezeka kutoka asilimia Saba kwenye utafiti wa kuanzia mwaka 2003 hadi 2006.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC Yury Fedotov amesema kati ya asilimia 15 hadi 20 ya waliosafirishwa ni watoto wa kike, wavulana asilimia 10 ambapo utafiti huo ulihusisha nchi 132.

UNODC imetaja hatua za kuepusha vitendo hivyo kuwa ni pamoja na kuwepo mfumo bora wa uhamiaji na kanuni thabiti za soko la ajira na mfumo bora wa haki.

Wahanga wa usafirishwaji huo, kwa mujibu wa ripoti hutumikishwa kazi, hupelekwa kwenye madanguro au hata kutakiwa kutolewa viungo vya ndani kwa ajili ya biashara.