UNAMID yaratibu kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia

10 Disemba 2012

Huko Darfur, Sudan, siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia zimefikia kilele leo ambayo ni siku ya kimataifa ya haki za binadamu, ambapo kampeni ya kupinga vitendo hivyo iliratibiwa na kikundi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika cha kulinda amani kwenye eneo hilo, UNAMID.

Kampeni ilianza tarehe 25 mwezi uliopita ambapo wanawake wa Darfur wakiwemo waliopoteza makazi yao, wanafunzi, wakunga, na wawakilishi kutoka vikundi vya kiraia na walemavu walikutana na kuunganisha sauti zao za kupinga ukatili wa kijinsia kwenye jamii zao.

Ujumbe wa siku ya leo ya haki za binadamu ni kwamba Sauti yako ina umuhimu ambapo washiriki wa kampeni hiyo wanawake kwa wanaume walifanya maonyesho ya sanaa kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Naibu Mkuu wa UNAMID Mohammed Yonis alisoma ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- Moon ambao ulitaka kukomeshwa kwa ukatili wa kijinsia.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud