UNESCO yafanya hafla ya kumuunga Malala mkono

10 Disemba 2012

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, leo limefanya hafla ya kumuunga mkono msichana wa Kipakistani, Yousufzai Malala, na elimu ya mtoto wa kike. Hafla hiyo ambayo imeandaliwa na UNESCO pamoja na serikali ya Pakistan, imefanyika kwenye makao makuu ya UNESCO mjini Paris, Ufaransa, sambamba na siku ya kimataifa ya haki za binadamu.

Dhamira ya hafla hiyo ni kuchagiza kasi ya hatua za kisiasa ambazo zitamhakikishia kila mtoto wa kike haki yake ya kupata elimu, na kuendeleza elimu ya mtoto wa kike kama suala la kipaumbele katika kufikia lengo la elimu kwa wote.

Hafla hiyo imeandaliwa kama ishara ya heshima kwa Malala Yousufzai, msichana jasiri mwenye umri wa miaka 15, ambaye alinusurika kifo baada ya kushambuliwa kwa risasi kwa sababu ya juhudi zake katika kupigania haki ya mtoto wa kike kuwa na elimu nchini Pakistan, licha ya WaTaliban kupiga marufuku elimu ya wasichana katika Bonde la Swatt anakotoka.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter