Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miezi sita baadaye, mahitaji bado ni mengi jimbo la Rakhine, Myanmar: UNHCR

Miezi sita baadaye, mahitaji bado ni mengi jimbo la Rakhine, Myanmar: UNHCR

Miezi sita baada ya ghasia za wenyewe kwa wenyewe kuzuka katika jimbo la Rakhine magharibi mwa Myanmar, yapata watu 115, 000 walolazimika kuhama makwao bado wanaishi katika mazingira yenye matatizo, kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, UNHCR. Shirika hilo limesema limesambaza vifaa vya misaada kwa takriban thuluthi mbili za jamii zilizoathirika, ingawa mahitaji bado ni mengi sana.

Zaidi ya watu 100 waliuawa na maelfu ya nyumba kuharibiwa katika machafuko ya miezi ya Juni, Agosti na Oktoba.

Kwa sasa, wengi wa watu hawawezi kurudi makwao kwa sababu ya uharibifu mwingi unaoendelea na hali tete, na wanakaa katika kambi. Kama sehemu ya mwitikio wa mashirika ya kutoa misaada ya dharura katika jimbo la Rakhine, UNHCR inaongoza katika juhudi za kuwalinda, kuwapa makao, vifaa visivyo chakula na kudhibiti kambi wanamokaa. Msemaji wa UNHCR, Adrian Edwards, amesema misaada yao inalenga jamii zote zilizoathiriwa kulingana na mahitaji yao.

(SAUTI YA ADRIAN EDWARDS)