Mtandao wa intaneti wakatika kwenye mkutano wa kimataifa wa mawasiliano

6 Disemba 2012

Mawasiliano ya mtandao na moja ya tovuti za shirika la kimataifa la mawasiliano, ITU yalikatika kwa saa mbili na kusababisha mkanganyiko mkubwa miongoni mwa washiriki na wafuatiliaji wa mkutano wa kimataifa wa mawasiliano huko Dubai.

Kukatika kwa mawasiliano ya intaneti kulisababisha washiriki na wafuatiliaji kushindwa kupata nyaraka muhimu kutoka kwenye mtandao kwa kuwa mkutano huo hautumii makaratasi bali nyaraka zote muhimu ziko kwenye tovuti.

Taarifa ya ITU inasema kutokana na hali hiyo kikao cha kamati ya moja kililazimika kuchelewa kuanza na imetaja chanzo kuwa ni kuzidiwa kwa uwezo wa mtandao huo kutokana na watu wengi kufuatilia mkutano kupitia mtandao wa intaneti.

Hata hivyo akizungumzia tukio hilo Katibu Mkuu wa ITU Dkt. Hamadoun Touré ametupia lawama baadhi ya vikundi alivyodai kuingilia mtandao huo kwa lengo la kuzuia watu wengine kufuatilia mkutano huo.