Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bei ya chakula iliendelea kushuka mwezi Novemba: FAO

Bei ya chakula iliendelea kushuka mwezi Novemba: FAO

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO limesema wastani wa bei ya chakula umeendelea kushuka ambapo kwa mwezi uliopita wa Novemba ulishuka kwa asilimia Moja nukta Tano, ikilinganishwa na mwezi uliotangulia.

Ripoti ya FAO kuhusu bei za chakula inaonyesha kuwa bei ya kapu la chakula ilishuka kwa pointi Tatu na kufikia pointi 211 ikilinganishwa na mwezi Oktoba, kiwango ambacho ni cha chini zaidi kuwahi kufikiwa tangu mwezi Juni mwaka 2012.

FAO inasema bei za kimataifa zinaonyesha kushuka kwa kiasi kikubwa kwa bei ya sukari, ikifuatiwa na mafuta ya kupikia na nafaka.

Hata hivyo bei za bidhaa za maziwa hazikupungua.

Ikilinganishwa kwa miaka, FAO inasema kuwa thamani ya kipimo cha mwezi Novemba ni karibu chini zaidi kwa asilimia Tatu ikilinganishwa na mwaka mmoja uliopita.