Wakimbizi wa kipalestina waomba UNRWA isisitishe operesheni zake huko Syria

6 Disemba 2012

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada na usalama kwa wapalestina, UNRWA, Filippo Grandi amekagua operesheni za shirika hilo huko Yarmouk, Syria ambako wafanyakazi 3,700 wanaendelea kutoa huduma za kijamii licha ya mzozo unaoendelea.

Huduma hizo ikiwemo elimu na afya ni kwa ajili ya zaidi ya wakimbizi 500,000 wa kipalestina ambapo pia wafanyakazi hao wanashughulikia mahitaji mengine ya kibinadamu yatokanayo na mgogoro unaoendelea nchini Syria.

Baada ya mazungumzo yake na wafanyakazi na wakimbizi huyo Yarmouk, Bwana Grandi amewahakikishia kuwa katika mashauriano yake na serikali ya Syria na hata jumuiya ya kimataifa ataendelea kusisitiza mambo makuu matatu ambayo ni ulinzi kwa wakimbizi wa kipalestina na raia wengine, kutoshambuliwa majengo ya Umoja wa Mataifa na UNRWA na mazingira yawepo ili misaada ya kibinadamu iweze kuwafikia wahusika.

Vijana wa kipalestina wanaoishi ukimbizini Syria nao walimweleza Bwana Grandi kuchoshwa na kuathirika kwao kisaikolojia na mzozo unaoendelea na kuomba jumuiya ya kimataifa kuongeza maradufu jitihada za kutatua mzozo huo na UNRWA iendeleze operesheni zake za usaidizi wa kibinadamu.