Kuwait na Iraq zina fursa nzuri zaidi za kuimarisha uhusiano wao: Ban

5 Disemba 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliyeko ziarani Mashariki ya Kati, hii leo alitembelea Kuwait ambako ameeleza kutiwa moyo na maendeleo ya uhusiano kati ya nchi na Iraq, uhusiano ambao amesema unazidi kuimarika.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa Kuwait, Kuwait City, Bwana Ban amesema anaamini kuwa nchi mbili hizo zina fursa ya kihistoria ambayo inawezesha Iraq na Kuwait kusahau yaliyopita na kuanzisha enzi mpya ya ushirikiano.

Bwana Ban amesema yeye binafsi amejizatiti kuona uhusiano ulioharibiwa na kitendo cha Iraq kuvamia Kuwaiti mwaka 1990, unarejea katika hali ya kawaida na kuona Iraq ikitekeleza wajibu wake wa kulipa fidia Kuwait.

Mwaka 1991 baada ya Iraq kuvamia Kuwait, Umoja wa Mataifa ulianzisha Tume ya Fidia, UNCC ambayo inashughulikia malipo kwa wadai waliopata hasara kutokana na uvamizi huo ambapo hadi sasa imeshatoa dola Bilioni 37 nukta Saba kwa wadai zaidi ya Milioni Moja na Nusu wakiwemo watu binafsi, mashirika ya ndani na ya kimataifa pamoja na serikali.

Wakati wa ziara hiyo nchini Kuwait, Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alikuwa na mazungumzo na Mkuu wa nchi hiyo Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah, ambaye walijadili masuala kadhaa ya kikanda ikiwemo matumaini ya amani Mashariki ya Kati an mgogoro unaoendelea nchini Syria.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter