UNICEF yalaani shambulio la jana dhidi ya shule huko Damascus

5 Disemba 2012

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limelaani shambulio la jana kwenye shule moja iliyoko karibu na mji mkuu wa Syria Damascus ambalo lilisababisha mauaji ya wanafunzi kadhaa pamoja na mwalimu mmoja.

Mkurugenzi wa UNICEF kwa Ukanda wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini Maria Calivis amesema katika taarifa yake kuwa tangu kuanza kwa mapigano nchini Syria, vifaa vya shule vimekuwa vinaibwa, vinaharibiwa au vinachomwa moto.

Bi. Calivis amesema vitendo hivyo havikubaliki kwa kuwa maeneo ya shule ni maeneo ya amani na yanapaswa kubakia hivyo.

Amerejea wito wa UNICEF wa kuzitaka pande zote katika mgogoro nchini Syria kuzingatia wajibu wao kwa mujibu wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na kuhakikisha watoto wanalindwa wakati wote.