Uwanja wa ndege wa Goma waanza tena kutoa huduma: UM

5 Disemba 2012

Umoja wa Mataifa umesema Uwanja wa ndege wa Goma, Mashariki wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, umefunguliwa leo na unatoa huduma baada ya kufungwa kufuatia waasi wa kikundi cha M23 kuingia na kusonga ndani ya mji huo mwezi uliopita.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky ametoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari mjini New York, Marekani.

Mamlaka za Congo zimetangaza kufunguliwa tena kwa uwanja wa ndege wa Goma hii leo, MONUSCO na washirika wake wa kutoa misaada ya kibinadamu wanashughulikia kusafirisha kwa ndege misaada ya kibinadamu ya dharura kwenda Goma. Halikadhalika Radio Okapi jana imeanza tena matangazo yake huko Kinshasa ambayo yamekuwa yakisika Kivu wakati wote.”

Kuhusu hali ya usalama, Bwana Nesirky amesema bado si nzuri katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini huko Mashariki mwa DRC.

Amesema kinachoendelea sasa huko Kivu Kaskazini baada ya kuondoka kwa waasi wa M23, jeshi la DRC linarejea eneo la Sake, Magharibi mwa Goma, wakati kule Kivu Kusini, kikundi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, MONUSCO kinasaidia operesheni za jeshi la DRC za kukabiliana na vikundi vyenye silaha kwenye maeneo ya Bunyakiri, Hombo, na Kilembwe.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter