Mamilioni ya watu hujitolea stadi na uwezo wao kusaidia wengine: UNV

5 Disemba 2012

Mpango wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa, UNV umesema kila mwaka mamilioni ya watu duniani kote hujitolea muda wao na stadi zao kubadili maisha ya watu wengine.

UNV imesema hayo leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kujitolea ambapo msemaji wake Jennifer Stapper amesema ni fursa ya kutoa shukrani kwa wafanyakazi wa kujitolea wanaotekeleza majukumu yao bila kutarajia malipo.

Stapper amesema siku ya leo ni fursa kwa kikundi hicho pia kutoa shukrani kwa wafanyakazi wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa wanaotoka zaidi ya nchi 130 na ambao wengi wao hutoka nchi zinazoendelea.

(SAUTI YA JENNIFER STAPPER)

Siku ya kimataifa ya kujitolea inatupatia fursa sisi UNV fursa ya kuwashukuru wafanyakazi wetu kujitolea wa Umoja wa Mataifa ambao wanachangia katika malengo ya Umoja wa Mataifa ya amani na maendeleo. Pia tunachukua fursa hii kuwashukuru wafanyakazi wengine wa kujitolea duniani kote pengine hata wewe ambao huleta mabadiliko katika makazi yao na jamii zao.”

Siku ya Umoja wa Mataifa ya kujitolea ilianzishwa mwaka 1985 kwa lengo la kutambua nafasi kubwa ya kujitolea katika kubadili maisha.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter