Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Biashara inayowajibika ni ile inayojali haki za binadamu: UM

Biashara inayowajibika ni ile inayojali haki za binadamu: UM

Mkuu wa Ofisi ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Navi Pillay amezitaka serikali kuongeza jitihada zaidi kushughulikia vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye sekta ya biashara vilivyosababisha na kuendeleza mdororo wa sasa wa uchumi.

Akizungumza mjini Geneva, Uswisi kwenye kongamano la ngazi ya juu linaloangalia uhusiano kati ya maendeleo ya sekta ya biashara na haki za binadamu, Bi. Pillay amesema matakwa ya uhuru zaidi wa kisiasa yamekuwa yakienda sambamba na matakwa ya utawala wa kisheria kwenye sekta zote ikiwemo ile biashara na sekta binafsi.

Amesema sheria ya haki ya binadamu ya kimataifa inahitaji serikali kuwalinda raia dhidi ya vitendo vinavyokiuka haki zao ikiwemo vile vinavyofanywa na sekta ya biashara na ya fedha.

Watu wanataka  uhuru; Uhuru dhidi ya hofu na waweze kutosheka, huu ni wajibu mkubwa kwa watawala. Wat wanadai  utawala wa kisheria ubane pande zote hata kwenye sekta ya uchumi.  Wanadai utu, ambao ni kitovu cha lengo kuu la mifumo yetu ya kiuchumi na kisiasa. Sekta ya biashara inayowajibika inataka sekta hiyo itekeleze majukumu yake huku ikiheshimu haki za binadamu, kudhihirisha kuwa ustawi wa muda mrefu wa sekta ya biashara unategemea zaidi ustawi wa jamii. Haya si mambo mapya kufanywa na serikali; yamekuwa sehemu ya mfumo wa haki za binadamu za kimataifa kwa miongo kadhaa.”

Kongamano hilo linamulika utekelezaji wa mwongozo uliokubalika kimataifa wa misingi ya Biashara na Haki za Binadamu, unaosaidia kuzuia na kushughulikia madhara ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika sekta ya biashara.