Hali mbaya ya usalama Syria: UM kusitisha baadhi ya shughuli zake

3 Disemba 2012

Umoja wa Mataifa umesema unasitisha baadhi ya shughuli zake nchini Syria pamoja na kuondoa watendaji wake ambao si lazima wawepo nchini humo kutokana na kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama.

Msemaji wa umoja huo Martin Nesirky amesema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini New York, Marekani hii leo akikariri Idara ya Usalama na Ulinzi ya umoja huo.

Tunaweza kuthibitisha kuwa Umoja wa Mataifa nchini Syria utaondoa mara moja wafanyakazi wake wa kimataifa wasio wa lazima nchini humo, na kadri hali itakavyobadilika, Umoja wa Mataifa unatathmini operesheni zake na kuangalia watendaji ambao wanapaswa kutekeleza shughuli hizo. Naweza pia kuwaeleza kwamba Umoja wa Mataifa utasitisha kazi zake nchini humo hadi itakapotangazwa tena.”

Halikadhalika Bwana Nesirky amesema hali ya kuzorota kwa usalama nchini Syria ilielezwa bayana hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- Moon na hata mjumbe wa pamoja wa umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za kiarabu Lakhdar Brahimi alipohutubia Baraza la Kuu na lile la Usalama la Umoja wa Mataifa.