Pande zinazozozana Yemen zaahidi kutoandikisha watoto jeshini: Zerrougui

3 Disemba 2012

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye masuala ya watoto na mizozo ya kivita, Leila Zerrougui amesema pande zinazozona nchini Yemen zimekubaliana kuachana na mpango wa kuandikisha watoto kwenye majeshi yao.

Kauli hiyo ya Zerrougui ameitoa leo alipozungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani kufuatia ziara yake nchini Yemen.

Ameielezea ziara yake hiyo ya siku tatu nchini Yemen iliyotokana na mwaliko wa serikali, kuwa ilikuwa ya manufaa kwa kuwa aliweza kukutana na pande zote zinazohusika na uandikishaji wa watoto kwenye majeshi.

"Kutokana na mgogoro wa mwaka 2001, pande zote kwenye mgogoro huo ziliandikisha watoto, kwa hiyo uamuzi huo kwangu ni muhimu sana. Kuna pande nne zilizoorodheswa; Jeshi la Yemen, kikosi cha kwanza cha jeshi, Al Houti na wanamgambo wa kikabila. Kwetu sisi ilikuwa muhimu kupata ahadi yao na kuanza kuandaa mpango wa kuanza kutekeleza ahadi yao.”

Kuhusu hali ya Yemen, Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema bado ni ya mashaka na mgogoro na ukosefu wa utulivu nchini humo vinaendelea kuwaathiri watoto.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter