UNAMID yasaidia harakati za kupambana na homa ya manjano Darfur

3 Disemba 2012

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wa usaidizi huko Darfur, UNAMID umetia shime katika juhudi za kupambana na homa ya manjano kwenye jimbo hilo ambapo imesaidia usafirishaji wa vifaa kwenda maeneo ambako kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo inatekelezwa.

Kaimu Mkuu wa UNAMID Aïchatou Mindaoudou amesema ofisi yake inajisikia faraja kushiriki katika mpango huo wa kuokoa maisha, ambapo pindi baada ya shehena ya kwanza na nyingine za chanjo zilipowasili kutoka Khartoum Sudan, walisafirisha kwa ndege kwenda maeneo ya Kaskazini, Mashariki, Magharibi na kati ya Darfur.

Kampeni ya chanjo ilianza mwezi uliopita tangu ugonjwa huo uripotiwe mwezi Septemba ambapo UNAMID pia imetoa usaidizi wa kimatibabu, vifaa kama vile jenereta na msaada wa kiufundi.

Kwa sasa UNAMID inajiandaa kusafirisha dawa za kuua wadudu kwa ajili ya kudhibiti vimelea kwenye kambi za watu waliopoteza makazi yao kwenye mji wa Zalingei, Darfur ya kati.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter