Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mikakati ya Bangladesh ya kujiandaa dhidi ya majanga ni mfano wa kuigwa: UM

Mikakati ya Bangladesh ya kujiandaa dhidi ya majanga ni mfano wa kuigwa: UM

Mratibu Mkuu wa Masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa Valerie Amos ametembelea Bangladesh kujionea jinsi nchi hiyo inavyojiandaa dhidi ya majanga ambapo amesema mikakati ya nchi hiyo ni mfano wa kuigwa.

Bi. Amos ametaja mikakati hiyo ni pamoja na nchi hiyo kuwekeza mbinu za kujiandaa dhidi ya majanga kwa wananchi wenyewe kutokana na nchi hiyo kuwa hatarini zaidi kukumbwa na vimbunga na mafuriko kila mwaka.

Mathalani amesema Bangladesh imewapatia mafunzo wanajamii Elfu 25 wa kujitolea pindi kimbunga au mafuriko yanatokea, hatua ambayo amesema si gharama kubwa lakini inaokoa maisha na hivyo nchi nyingine zijifunze kutoka kwa Bangladesh.

Tangu kukumbwa na kimbunga kikali mwaka 1991 kilichosababisha vifo vya watu zaidi ya Laki Moja na Elfu Arobaini, Bangladesh imechukua hatua madhubuti kupunguza athari za majanga na kimbunga cha mwaka 2007, idadi ya vifo ilikuwa Elfu Nne.