Umoja wa Mataifa utaendelea kuunga mkono Intaneti huria: Ban

3 Disemba 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kuunga mkono uhuru wa kujieleza kupitia mtando wa intaneti, akiongeza kuwa teknolojia ya habari na mawasiliano inazidi kubadilisha ulimwengu kwa kuwafungulia watu milango ya ufanisi, kuokoa maisha, kutoa elimu na kuwapa uwezo zaidi.

Akitaja mfano wa mabadiliko ya kisiasa katika nchi za Kiarabu, Bwana Ban amesema mabadiliko hayo yalikuwa ishara kuwa teknolojia ya ICT inaweza kuwapa watu uwezo wa kujieleza kuhusu matakwa na haki zao, pamoja na kudai uwajibikaji.

Bwana Ban amesema hayo katika ujumbe wake kwa njia ya video ya mtandao wa YouTube kwa kongamano la kimataifa kuhusu teknolojia ya habari na mawasiliano, ambalo limeanza leo mjini Dubai, ambapo amesema dhamira kuu ya midahalo ya kongamano hilo ni kuhakikisha kufurahia kwa matunda ya teknolojia ya habari na mawasiliano kwa wote, ikiwemo thuluthi tatu za watu duniani wasio na intaneti.