Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jitihada za kuwapatia walemavu haki zao ziimarishwe: Ban

Jitihada za kuwapatia walemavu haki zao ziimarishwe: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema hatua zaidi zichukuliwe kutekeleza ahadi nzuri zinazotolewa kwa ajili ya kuimarisha maisha ya zaidi ya watu bilioni Moja wanaoishi na ulemavu duniani kote.

Ban katika ujumbe wake wa siku ya walemavu duniani hii leo, amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa changamoto kubwa hivi sasa ni kuhakikisha kundi hilo linapata haki sawa katika huduma wanazohitaji kama ilivyokubaliwa kwenye mkutano wa Rio + 20 ya kwamba mustakhabali wa dunia unategemea jinsi mtu anavyopata mahitaji yake.

Wakati ujumbe wa mwaka huu ni Ondoa vikwazo na jenga jamii jumuishi kwa wote, Bwana Ban amesema vikwazo viko vya aina nyingi ikiwemo mazingira ambamo walemavu wanaishi, teknolojia ya mawasiliano, pamoja na vile vinavyosababishwa na sera, mtazamo wa kijamii na hata ubaguzi.

Amekumbusha Jumuiya ya kimataifa kushirikiana kufanikisha malengo ya mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu ambao mpaka sasa theluthi mbili za nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimesharidhia.