Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Palestina yakubaliwa hadhi ya uangalizi ndani ya Baraza Kuu la UM

Palestina yakubaliwa hadhi ya uangalizi ndani ya Baraza Kuu la UM

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, limepitisha azimio linaloipatia Palestina hadhi ya uangalizi bila haki ya kupiga kura katika Baraza hilo, azimio ambalo limepitishwa leo siku ambayo ni ya kimataifa ya kusimama bega kwa bega na Palestina.

Kazi ya kupiga kura imefanyika Alhamisi jioni ya leo, ambapo nchi 138 ziliunga mkono huku Tisa zikipinga na nchi 41 zikijiondoa katika upigaji kura.

Nchi zilizopinga azimio hilo ni pamoja na Marekani na Israeli huku Uingereza na Hungary zikiwa miongoni mwa nchi ambazo hazikuonyesha msimamo wowote.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema azimio hilo limetoa fursa ya kuendeleza mchakato wa amani kati ya Israeli na Palestina na kwamba siku zote yeye msimamo wake umekuwa wa wazi ya kuwa wapalestina wana haki ya kuwa na taifa lao na Israeli nayo pia ina haki ya kuishi kwa amani.

Bwana Ban amesema yeye kwa upande wake atatekeleza kile anachopaswa kufanya kwa mujibu wa azimio hilo na amezitaka Palestina na Israeli kuendeleza jitihada za amani kwa manufaa ya wananchi wao.

(SAUTI YA BAN)

Mapema akiwasilisha rasimu ya azimio hilo, Mwakilishi wa kudumu wa Sudan katika Umoja wa Mataifa Daffa-Alla Elhag Ali Osman amesema azimio hilo ni la kihistoria na ni mwendelezo wa misingi ya katiba iliyoanzisha Umoja wa Mataifa.