Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado kuna changamoto kufuatilia uzalishaji wa nyuklia Syria, Iran na DPRK: IAEA

Bado kuna changamoto kufuatilia uzalishaji wa nyuklia Syria, Iran na DPRK: IAEA

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la nguvu za atomiki la Umoja wa Mataifa, IAEA, Yukiya Amano leo ametoa ripoti mbele ya bodi ya magavana wa shirika hilo huko Vienna, Austria kuhusu ufuatiliaji wa mipango ya nyuklia huko Iran, Syria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK na kueleza wasiwasi wake juu ya mipango ya nyuklia ya nchi hiyo.

Mathalani amesema shirika lake lina wasiwasi mkubwa kuhusu mpango wa nyuklia wa DPRK kwa kuwa kwa zaidi ya miaka mitatu sasa hawajaweza kufuatilia usalama wa miradi hiyo kwenye maeneo ya mitambo nchini humo zaidi ya kufuatilia kwa kutumia setilaiti.

Kuhusu Iran amesema nako hawajaweza kupata kibali cha kwenda kukagua mtambo wa Parchin ambao picha za setilatili zinaonyesha harakati za ujenzi zikiendelea.

Akizungumzia Syria, Mkuu huyo wa IAEA amerejelea ombi lake kwa serikali ya nchi hiyo la kutoa ushirikiano juu ya masuala ambayo hayajapatiwa ufumbuzi kuhusu mtambo wa nyuklia la Dair Alzour na maeneo mengine.

Mkutano huo wa bodi ya magavana wa IAEA unakutana kujadili hatua za shirika hilo za kufuatilia masuala ya usalama wa nyuklia ikiwemo matumizi salama ya teknolojia hiyo.