UM kumtunuku Askofu Desmond Tutu kwa kuchangia haki za binadamu

28 Novemba 2012

Mshindi wa tuzo ya Nobel na mwanaharakati wa haki za Binadamu, Askofu Desmond Tutu, atakabidhiwa tuzo ya heshima kwa mchango wake katika kujenga desturi ya haki za binadamu kote duniani, limetangaza leo Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO.

Askofu Tutu alichaguliwa kuipokea tuzo ya mwaka huu ya UNESCO/Bilbao, kwa mchango wake wa kupongezwa katika kujenga Afrika Kusini yenye demokrasia na isiyo na ubaguzi wa rangi, na kwa mchango wake mkubwa kama mwenyekiti wa tume ya ukweli na maridhiano ya Afrika Kusini katika ukarabati wa kitaifa, ambao umekuwa wa kuigwa na jamii zote zinazoondoka kwenye migogoro, limesema shirika la UNESCO kwenye tovuti yake.

Tuzo hiyo inatambua uanaharakati wake, hususan na vijana, katika kuendeleza kutokuwepo ghasia na kupinga aina zote za ubaguzi na kutotenda haki. Jopo la wateuzi pia limetaja kwa msisitizo mchango wa Bwana Tutu kwa kazi ya Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu, yakiwemo kuendeleza desturi ya haki za binadamu.

Bwana Tutu atakabidhiwa tuzo hiyo na Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova kwenye makao yake mjini Paris Ufaransa, mnamo Disemba 10, ambayo ni siku ya kimataifa ya haki za binadamu.