Mjumbe wa UM asikitishwa na mashambulizi ya kutisha huko Iraq

28 Novemba 2012

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Martin Kobler ameeleza kusikitishwa kwake na mfululizo wa mashambulizi yanayoendelea dhidi ya raia wasio na hatia ikiwemo waumini nchini humo.

Kobler amesema vitendo hivyo visivyo vya kibinadamu vinaongezea machungu na mateso ambayo tayari raia wasio na hatia wanakumbana nayo nchini Iraq.

Taarifa ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi nchini humo UNAMI unaoongozwa na Bwana Koble, imemkariri akiwapa pole wafiwa na uponaji wa haraka kwa waliojeruhiwa.

Habari zinasema mashambulizi hayo matatu tofauti yalitokea karibu na misikiti ya waislamu wa madhehebu ya Shia iliyopo kaskazini na kaskazini-mashariki mwa mji mkuu Baghdad ambapo watu 19 waliuawa na makumi kadhaa walijeruhiwa.