Baraza la Usalama la UM lapitisha azimio lingine kuhusu DRC: Lalaani vitendo vya M23

28 Novemba 2012

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio ambalo pamoja na mambo mengine linalaani kitendo cha kikundi cha waasi cha M23 cha kutaka kujaribu kuunda mamlaka isiyo halali na kupuuza serikali ya serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Azimio hilo limepitishwa bila kupingwa na wajumbe wote 15 wa Baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa katika kikao chake kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini New York, Marekani, ambapo pia linalaani mashambulio yanayofanywa na waasi hao dhidi ya raia, walinzi wa amani na watumishi wanaotoa misaada ya kibinadamu.

Halikadhalika, azimio hilo linaunga mkono hatua za katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, pamoja na zile za viongozi wa nchi za maziwa makuu, SADC na Umoja wa Afrika za kurejesha amani na usalama huko mashariki mwa DRC huku likitaka msaada wowote wa kigeni dhidi ya waasi wa M23 usitishwe mara moja.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na wawakilishi wa Rwanda na Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo katika Umoja wa Mataifa.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter