Lebanon inahitaji fedha zaidi kuhudumia wakimbizi wa Syria: UM

28 Novemba 2012

Mratibu Mkuu wa Masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa Bi. Valerie Amos amesema kuna umuhimu wa jumuiya ya kimataifa kuendelea kusaidia Lebanon wakati huu ambapo inatoa hifadhi kwa maelfu ya wakimbizi wa Syria wanaokimbia mapigano nchini mwao.

Bi. Amos amesema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Beirut, Lebanon baada ya mazungumzo yake na viongozi wa serikali pamoja na baadhi ya wakimbizi wa Syria, mkutano ambapo pia ulihudhuriwa na waziri wa ustawi wa jamii wa Lebanon, Wael Abu Faour.

Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake utaendelea kushirikiana na Lebanon huku ikihamasisha msaada zaidi kwa kuzingatia mpango wa msaada wa Umoja wa Mataifa na ule wa serikali hiyo.

Nilipata fursa ya kujadiliana na maafisa wa serikali juu ya changamoto kwa serikali inayopata hasa katika kutoa huduma ya afya na elimu kwa kuzingatia idadi kubwa ya wakimbizi wanaohudimiwa na umuhimu wa jumuiya ya kimataifa kuipatia serikali ya Lebanon fedha ili kuunga mpango wake wa kuhudumia wakimbizi. Sisi katika Umoja wa Mataifa tutaendelea kusaidia kadri tunavyoweza na pia tutaendelea kuwa watetezi kwa Lebanon pamoja na washirika wengine wa Jumuiya ya kimataifa.”

Halikadhalika, Bi Amos amesema wakati wa ziara yake alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wakimbizi waliomweleza madhila waliyopata ikiwemo mwanamke mmoja aliyesema alishuhudia mume wake akiteswa hadi kufa.