Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban na Üzümcü waomba mataifa yote kujiunga na mkataba wa kupinga silaha za kemikali

Ban na Üzümcü waomba mataifa yote kujiunga na mkataba wa kupinga silaha za kemikali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kupinga Silaha za Kemikali, Ahmet Üzümcü, leo wametoa waraka wa pamoja kwa nchi nane zisizo wanachama wa mkataba kuhusu silaha za kemikali.

Waraka wa viongozi hao wawili unasisitiza umuhimu wa mataifa yote kutia saini mkataba wa kupinga silaha za kemikali, kama sehemu muhimu ya kuwa na ulimwengu usio kuwa na silaha za kemikali. Wametoa wito kwa nchi hizo kujiunga na mkataba huo bila kuchelewa.

Mkataba wa kuoinga silaha za kemikali una nchi 188 wanachama kwa sasa, zikiwakilisha zaidi ya asilimia 98 ya idadi ya watu kote duniani na sekta ya kemikali. Nchi ambazo hazijajiunga na mkataba huo ni Angola, Misri, Israel, Myanmar, Korea Kaskazini, Somalia, Sudan Kusini na Syria.

Waraka huo unasema kuwa kuongezeka kwa uanachama wa mkataba huo ni ushuhuda kuwa kupinga kuendeleza, kuzalisha, kulimbikiza na matumizi ya silaha za kemikali sasa ni desturi ya ulimwengu mzima.