Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan itafute suluhisho la kudumu kwa raia waliopoteza makazi ndani ya nchi yao: UM

Sudan itafute suluhisho la kudumu kwa raia waliopoteza makazi ndani ya nchi yao: UM

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu kwa wakimbizi wa ndani Chaloka Beyani hii leo ameitaka serikali ya Sudan kuongeza jitihada za kupatia suluhisho la kudumu raia wake kwenye maeneo mbali mbali nchini humo waliopoteza makazi.

Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku Tisa nchini Sudan iliyomkutanisha na watu kutoka pande mbali mbali nchini humo, Beyani amesema serikali hiyo ishughulikie masuala ya usalama, chakula, malazi, makazi, afya elimu na maji pamoja na njia za kuwezesha wakimbizi hao wa ndani kujipatia kipato.

Hata hivyo amesema jitihada za pamoja ni muhimu ili kufanikisha msaada na ulinzi huo huku akiongezea suala la suluhisho jipya la kisiasa na kuweka mazingira stahili kuhakikisha makubaliano yaliyokwishatiwa saini yanatekelezwa.

Kuhusu watu wenye asili ya Sudan Kusini, Bwana Beyani ameisihi serikali ya Sudan kuendeleza utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu kwa kuhakikisha watu hao hawanyanyaswi na haki zao hazikiukwi huku akiitaka iweke mazingira rafiki na serikali ya Sudan kwa watu hao kurejea makwao kwa hiari.

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR zinaoyesha kuwa nchini Sudan kuna takribani watu Milioni Mbili na Nusu waliopoteza makazi yao kwenye maeneo mbali mbali kutokana na ghasia huko Darfur, jimbo la Blue Nite na Kordofan Kusini.