Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Japan isikilize sauti za wananchi baada ya janga la nyuklia: Grover

Japan isikilize sauti za wananchi baada ya janga la nyuklia: Grover

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu upataji wa haki ya afya, Anand Grover amehitimisha ziara yake ya takribani wiki mbili huko Japan na kusisitiza umuhimu wa kufuatilia madhara ya miali ya nyuklia iliyotokana na ajali ya Fukushima kwa binadamu na wananchi wenyewe kushiriki kuhakikisha wanapata haki hiyo.

Hata hivyo Grover amepongeza jitihada za serikali ya Japani za kusimamia tafiti za afya huko Fukushima, huku akiitaka ipanue wigo kwenye maeneo yote yaliyokumbwa na miali ya nyuklia ya ajali hiyo pamoja na madhara ya kiafya ya muda mrefu kwa binadamu.

Amegusia wasiwasi unaowakumba wananchi waliodhurika na miali hiyo ya kwamba hawana uamuzi wa kile kinachowaumiza na kutaka serikali ya Japan kutathmini uhusiano kati ya haki ya afya kwa watu hao na hatua zilizochukuliwa baada ya ajali hiyo mbaya zaidi ya nyuklia kuwahi kusababisha na binadamu nchini humo.

Wakati wa ziara hiyo Grover alikutana na watu wa makund mbali mbali wakiwemo maafisa kutoka taasisi za serikali, kiraia, madaktari, wataalamu wa sheria, wawakilishi wa jamii na waathirika wa ajali ya Fukushima.

Ripoti yake ataiwasilisha kwenye kikao kijacho cha baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kitakachofanyika mwezi Juni