UNAMID yasaidia sekta ya elimu huko Darfur Kaskazini

26 Novemba 2012

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika huko Darfur, UNAMID umeshiriki katika kuleta maendeleo ya kielimu kwenye eneo hilo kwa kuipatia wizara ya Elimu ya Darfur Kaskazini mahema 12 yatakayokuwa madarasa kwa wafugaji wanaohamahama kwenye vitongoji vitano vya eneo hilo.

Taarifa ya UNAMID imesema kuwa msaada huo ni sehemu ya miradi ya kuleta mabadiliko ya haraka kwa jamii QIP inayotekelezwa na ofisi hiyo na unafuatia ombi la jamii hizo za wafugaji la vifaa ili watoto wao waweze kwenda shule ambapo mahema hayo yatakuwa ni mazingira bora zaidi ya kusomea kwa maelfu ya watoto na walimu wao kwenye vitongoji vya El Waha, Serif, Saraf Omra, Kabkabiya na El Cuma.

Kamishna wa Tume ya misaada ya kibinadamu kwa eneo la Darfur Kaskazini Ibrahim Ahmed Hamid ameishukuru UNAMID kwa msaada huo na kuomba ujumbe huo pia kupanua wigo wa stadi zaidi za kuwajengea uwezo wafugaji hao wanaohamahama wakiwemo wavulana, wasichana na hata wazee.

Kwa mujibu wa UNAMID, hadi sasa imeshatekeleza zaidi ya miradi 500 ya QIP kwa ajili ya jamii mbali mbali huko Darfur.