Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wa UM kuelekea Bahrain kuangalia ukiukwaji wa haki za binadamu

Ujumbe wa UM kuelekea Bahrain kuangalia ukiukwaji wa haki za binadamu

Jopo la Umoja wa Mataifa la kutathmini haki za binadamu, mapema mwezi ujao litakwenda Bahrain kwa mwaliko wa serikali ya nchi hiyo kujadili mfumo wa mahakama nchini humo na uwajibikaji kwa vitendo vya sasa na vilivyopita vya ukikwaji wa haki za binadamu.

Msemaji wa Tume ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Rupert Colville amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuwa ziara hiyo iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu inafuatia ziara kama hiyo iliyofanyika mwezi Disemba mwaka jana.

Wataalamu hao wanne wakiwa Bahrain watakutana na viongozi wa kiserikali na wa kiraia pamoja na wananchi wa kawaida ambapo watajadili hatua za serikali katika kutekeleza mapendekezo ya tume huru ya uchunguzi nchini humo na yale yaliyopitishwa wakati wa kikao cha kutathmini haki binadamu Bahrain kilichofanyika Geneva.

Wakati huo huo Colville amemkariri Mkuu wa Tume hiyo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Navi Pillay akishutumu kitendo cha serikali ya Bahrain kubatilisha uraia watu 31 kwa madai ya kuhatarisha usalama wa Taifa, kitendo ambacho kinaweza kuwafanya watu 16 kati yao kutokuwa na uraia wa nchi yoyote.

Bi.Pillay ameitaka Bahrain kuangalia upya uamuzi huo ambao amesema ni ukiukwaji wa kifungu 15 cha mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu kinachosema kila mtu ana haki ya uraia.