Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay asikitishwa na kurejeshwa kwa adhabu ya kifo Afghanistan

Pillay asikitishwa na kurejeshwa kwa adhabu ya kifo Afghanistan

Kamishna Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za binadamu, Navi Pillay ameeleza wasiwasi wake mkubwa juu ya hukumu ya kifo dhidi ya wafungwa 14 nchini Afghanistani iliyotekelezwa tarehe 20 na 21 mwezi huuu.

Taarifa ya Tume ya haki za binadamu inasema kuwa Rais Hamid Karzai ameripotiwa kuidhinisha adhabu ya kifo kwa wafungwa hao baada ya kesi zao kuwa miongoni mwa kesi 250 zilizopitiwa upya tume ya Rais.

Bi. Pillay ameeleza kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kwa mujibu wa sheria za Afghanistan, hukumu ya kifo ni kwa ajili ya makosa makubwa zaidi ya uhalifu na inapaswa kutekelezwa baada ya mchakato mrefu na wa kina wa mahakama.

Hivyo basi amemtaka Rais Karzai kuonyesha kuwa utawala wa kisheria unaweza pia kuimarishwa kwa kuonyesha ubinadamu na kusamehe na kwa kufanya hivyo Afghanistan itaungana na ulimwengu mzima katika kupinga adhabu ya kifo.