Uimarishaji kilimo Haiti wahitaji dola Milioni 74: FAO

23 Novemba 2012

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO na serikali ya Haiti zinatafuta dola Milioni 74 katika kipindi cha mwaka mmoja ujao kwa ajili ya kurekebisha sekta ya kilimo nchini humo iliyoharibiwa na mfululizo wa majanga ya asili tangu kuanza kwa mwaka huu.

Majanga hayo ni vimbunga Sandy na Isaac pamoja na ukame ambayo yamefanya Haiti kutarajia hasara ya dola Milioni 254 kwa kuwa ekari zaidi ya Elfu 90 za mazao zimeharibiwa, mifugo Elfu 64 kufa na hivyo kuweka watu zaidi ya Milioni Moja na Nusu katika harati ya kupata utapiamlo mkali.

Takwimu hizo zimetolewa wakati Rais Michel Joseph Martelly wa Haiti alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo duniani, FAO Jose Graziano de Silva mjini Roma, Italia.

Katika mazungumzo hayo, FAO na serikali ya Haiti zimesema zinatafuta dola Milioni 74 katika kipindi cha mwaka mmoja ujao kusadia kurekebisha sekta ya kilimo iliyoharibiwa na vimbunga na ukame.

Bwana Da Silva ameongeza kuwa FAO itasaidia Haiti kwa kutoa msaada ya kimkakati itakayowezesha nchi hiyo kuondokana na tatizo sugu la ukosefu wa uhakika wa chakula na umaskini.