Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jitihada za Malala kutetea mtoto wa Kike ziendelezwe kwa kasi kubwa: UM

Jitihada za Malala kutetea mtoto wa Kike ziendelezwe kwa kasi kubwa: UM

Mkuu wa Tume ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Navi Pillay amesema mtoto Malala Yousfzai atakuwa ametendewa haki zaidi iwapo harakati zake za kutafuta haki ya elimu kwa mtoto wa kike zitaendelezwa zaidi ya kile kilichofanywa sasa baada ya yeye kunusurika kuuawa.

Katika taarifa yake kwa siku ya kimataifa ya kutokomeza aina zote za unyanyasaji dhidi ya wanawake tarehe 25 mwezi huu, Bi. Pillay amezungumzia kile kitokanacho na hatua ya Malala ya kutetea mtoto wa kike na kusema kuwa Malala alishambuliwa siyo kwa sababu tu yeye mwenyewe alitaka kupata elimu bali kwa sababu alikuwa anafanya kampeni kwa watoto wote wa kike kupata elimu kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu.

Kwa hivyo basi huku akimtakia Malala uponaji wa haraka, Bi Pillay ametaka kitendo cha Malala kujitolea uhai wake kisionekane kuwa ni maajabu kwa wiki sita au miezi sita tu bali kasi iongezeke kwa kile alichokianzisha cha kutetea haki ya elimu kwa mtoto wa kike .