Skip to main content

UNESCO yataka mauaji ya mwandishi wa habari huko Mexico yachunguzwe

UNESCO yataka mauaji ya mwandishi wa habari huko Mexico yachunguzwe

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Irina Bokova amelaani mauaji ya mwandishi wa habari Adrian Silva Moreno wa Mexico na kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu chanzo cha mauaji hayo na ya afisa wa zamani wa polisi Misray López González.

Bi. Bokova ambaye shirika lake lina wajibu wa kutetea uhuru wa vyombo vya habari amesema ni muhimu watuhumiwa wa mauaji hayo wakamatwe na wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.

Ametaka hatua thabiti zichukuliwe ili waandishi wa habari nchini Mexico waweze kutekeleza majukumu yao ambayo ni muhimu kwa kujenga demokrasia na utawala wa kisheria na kwamba haki ya msingi ya binadamu ya kujieleza inapaswa kulindwa.

Moreno aliripotiwa kuuawa tarehe 14 mwezi huu ndani ya gari lake wakati akijaribu kufuatilia madai ya wizi wa mafuta kutoka mabomba ya kusafirisha mafuta ya serikali kwenye mji wa Tehuacan.