Ban ashutumu shambulio dhidi ya basi huko Tel Aviv

21 Novemba 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- Moon ambaye yuko ziarani Mashariki ya Kati kupatia suluhu mzozo kwenye eneo hilo, ameshutumu vikali shambulio lililotokea leo kwenye basi moja huko Tel Aviv, Israel na kusababisha watu Kumi kujeruhiwa.

Msemaji wa Bwana Ban, amemkariri Katibu Mkuu huyo akielezea kusikitishwa na kushtushwa na taarifa za shambulio hilo la kigaidi na kusema hakuna mazingira yoyote ya kuhalalisha kitendo hicho.

Shambulio hilo limetokea wakati Bwana Ban akijitahidi kusuluhisha mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati ambapo tayari amezitaka pande zote husika kujizuia kufanya mapigano na kulinda raia.

Tayari Bwana Ban amekwenda Misri na jana alikuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na baadaye leo amepanga kukutana na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas mjini Ramallah kwenye ukingo wa magharibi wa mto Jordan.